Pinda: Vyama vijiandae kisaikolojia kwa matokeo..



Waziri Mkuu Mizengo PindaWaziri Mkuu Mizengo Pinda.


Dar es Salaam. Waziri Mkuu Mizengo Pinda amevitaka vyama vya siasa nchini kujiandaa kisaikolojia kuyapokea matokeo ya Uchaguzi Mkuu utaokaofanyika nchini, Jumapili ijayo.
Pinda alitoa rai hiyo jana wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la ghorofa 16, Victoria Place la Shirika la Nyumba Taifa (NHC) jijini Dar es Salaam.
Alisema vyama hivyo vilivyosimamisha wagombea katika uchaguzi huo wa rais, wabunge na madiwani, vinatakiwa kujiandaa kisaikolojia kupokea matokeo hayo yatakayotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), baada ya wananchi kupiga kura, huku vikitambua katika uchaguzi kuna ushindi na kushindwa.
“Lakini kubwa kwenye mashindano kuna mshindi na mshindwa, lazima tujiandae kisaikolojia, kushinda au kushindwa, mkikuta mmeshindana… Tume ya Taifa ya Uchaguzi itaeleza, lakini katika uchaguzi wa amani mshindi ni demokrasia,” alisema Pinda na kuongeza kuwa:
“Tuko katika lala salama ya kampeni, naamini kila mtu anaiona Oktoba 25 ilee; watu hatulali! Wacha siku ifike tupunguze kelele. Wenye msiba watalia, watakaozaa mtoto watafurahi. Jambo la msingi ni Watanzania wote tuliojiandikisha tujitokeze kwa wingi kupiga kura.”
Vilevile, aliwahimiza Watanzania kujitokeza kwa wingi kupiga kura na wakimaliza warudi nyumbani badala ya kusubiri vituoni kwa madai ya kulinda kura.
“Ukimaliza kupiga kura rudi nyumbani ukapumzike. Kuna lugha zinatolewa zikitaka wananchi kulinda, jamani kura zinalindwa na mawakala, huyo ndiyo atasema kama kuna tatizo,” alisema.
Kauli hiyo imekuja kabla ya uchaguzi huo utakaovishirikisha vyama vingi vya siasa kwa mara ya tano kufanyika nchini Oktoba 25, ambao utaiweka madarakani Serikali ya awamu ya tano.
Katika uchaguzi huo, mpambano mkali wa urais ni kati ya mgombea wa CCM, Dk John Magufuli, ambacho Pinda ni kada wake na wa Chadema, Edward Lowassa chini ya mwamvuli wa Ukawa. Wagombea hao ni kati ya wanane waliojitosa katika kinyang’iro hicho kumrithi Rais Jakaya Kikwete.
Awali Pinda alisema Serikali inatambua changamoto zinazolikabili shirika hilo kufikia malengo yake ya kujenga nyumba zinazofikia milioni tatu nchini.
Alisema Serikali inazifanyia kazi ikiwamo kuangalia namna ya kupunguza Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), na kwenye vifaa vya ujenzi ili shirika hilo liweze kujenga nyumba za makazi na biashara kwa gharama nafuu.
Aliziagiza halmashauri nchini kuhakikisha zinaandaa mipango ya uendelezaji wa miji yao, kutenga na kupima maeneo maalum kwa miradi ya ujenzi wa nyumba za kisasa za bei nafuu kwa ajili ya wananchi.
Vilevile, alizitaka wizara na taasisi binafsi na za umma kushirikiana na NHC kukabili mahitaji ya nyumba nafuu nchini.
Pinda alisema licha ya kustaafu wadhifa wake siku chache zijazo, atakuwa tayari kuisaidia NHC kwa ushauri ili iweze kufikia malengo.








SOURCE:Mwananchi













































Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

USAJILI WENYE MANUFAA EPL HADI SASA..