Serikali yasifia magazeti ya Mwananchi..




Dar es Salaam. Magazeti yanayochapishwa na kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) ya Mwananchi na The Citizen yametajwa kuwa vinara wa kuripoti habari za uchaguzi bila kuonyesha ushabiki wala upendeleo tofauti na mengine nchini.
Msemaji wa Serikali ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Assah Mwambene alitoa tathimini hiyo jana mbele ya jopo la waangalizi wa uchaguzi kutoka Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) katika mkutano uliowakutanisha wahariri na waandishi wa habari, uliolenga kubaini mwenendo wa vyombo vya habari katika kipindi hiki cha uchaguzi na changamoto zinavyokabiliana nazo.
Mwambene alifafanua kuwa kwa kiasi kikubwa Mwananchi na The Citizen yamejitahidi kuzingatia weledi katika uandishi wa habari za wagombea katika kipindi cha kampeni bila kuonyesha upendeleo kwa vyama vya siasa nchini.
Pamoja na magazeti ya MCL, Mwambene alilitaja gazeti la Serikali la Daily News kuwa limefanya kazi nzuri na kuripoti habari za vyama bila kujali umiliki wake.
“Magazeti yapo mengi lakini niweke wazi kuna magazeti matatu ambayo ni Daily News, Mwananchi na The Citizen yanaonyesha kufanya kazi bila upendeleo tena haya yanayomilikiwa na MCL yameonyesha weledi hata ukiangalia habari zake unaona wazi zinawatendea haki wagombea wa vyama vyote” alisema
Mwambene ametoa tathmini hiyo wakati ripoti ya nne ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) ikiendelea kuyataja magazeti ya MCL kwa kuandika habari za uchaguzi kwa kuzingatia weledi, bila upendeleo na kutoa nafasi kwa wananchi kuzungumza na wagombea wao.
Hiyo ni mara ya nne kwa MCT linalofuatilia la mwenendo wa vyombo vya habari katika kuandika habari za Uchaguzi Mkuu nchini kwa kutoa ripoti inayoonyesha magazeti ya Mwananchi na The Citizen yanaongoza kwa weledi.
Kwa mujibu wa ripoti ya MCT iliyotolewa jana, kati ya magazeti 15 yaliyokuwa yakifanyiwa utafiti, magazeti ya MCL yameongoza kwa kuzingatia weledi katika kuandika habari za uchaguzi bila upendeleo.





SOURCE:Mwananchi
























Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

USAJILI WENYE MANUFAA EPL HADI SASA..