Magazeti ya Mwananchi yaibuka tena kidedea uchaguzi...
Magazeti hayo yanayochapishwa na kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) yameibuka kidedea katika utafiti wa mwenendo wa vyombo vya habari katika kuandika habari za uchaguzi uliofanywa na Baraza la Habari Tanzania (MCL). Utafiti huo ulihusisha magazeti 15.
Mbali na magazeti ya Mwananchi na The Citizen, mengine yaliyohusika katika utafiti huo ni pamoja na Nipashe, Uhuru, Mzalendo, Tanzania Daima, Mtanzania, Rai Tanzania, Jambo Leo, Zanzibar Leo, Daily News, Sunday News, The Guardian, Habari Leo na Majira.
Taarifa ya MCT inasema kuwa licha ya utafiti huo kuhusisha magazeti, vyombo vingine vilivyokuwa vikifanyiwa uchunguzi ni televisheni na redio.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, utafiti huo pia uliangalia jinsi vyombo vya habari vinavyoandika habari za uchaguzi, ukiangalia mambo matatu ya msingi yanayoihusu jamii na Taifa, ambayo ni rushwa, jinsia na masuala ya Katiba.
Ripoti hiyo inasema kuwa katika kipindi cha wiki moja walichofanyia utafiti kati ya Oktoba 2 - 8, magazeti hayo yalikuwa yakitoa nafasi ya wananchi kuzungumza na wagombea.
Kwa upande wa The Citizen, ripoti hiyo inasema gazeti hilo lilichapisha habari za uchaguzi kwa asilimia 97 kwa usahihi na usawa bila upendeleo kwa chama chochote, vikiwamo vyama visivyotajwa mara kwa mara.
Ripoti hiyo inaongeza kuwa katika kipindi hicho, gazeti la Mwananchi kwa asilimia 98 lilichapisha habari zake kwa usawa, usahihi pasipo kukibeba chama chochote.
Inasema kuwa magazeti yote ya The Citizen na Mwananchi yalihakikisha kuwa habari zake zinagusa masuala muhimu ya kijamii na kitaifa katika kipindi cha kampeni, kama habari za elimu, maji, mafuta, gesi, ukuaji wa uchumi, jinsia, rushwa, kilimo na miundombinu..
“Katika wiki hii gazeti la Mwananchi lilikuwa na habari 92 za uchaguzi, ambazo hazikulenga kumuumiza mgombea wala chama chochote, ziliandikwa kwa usahihi na ukweli,” inasema ripoti hiyo.
Katika tafiti nne zilizotolewa wakati kampeni zikiendelea, magazeti ya Mwananchi na The Citizen yalikuwa yakikwepa kuandika habari za mtu mmoja badala yake ilitoa fursa ya wasemaji wengi kuzungumza kwenye habari moja.
Aidha tafiti hizo zilionyesha kuwa magazeti hayo yalijitahidi kuhakikisha yanawapa wanaotuhumiwa nafasi za kujibu tuhuma zao..
Maoni
Chapisha Maoni