RPC Arusha aonya makundi yanayotaka kufanya vurugu...
Kamanda wa Polisi mkoa Arusha, Liberatus Sabas.
Arusha. Kamanda wa Polisi mkoa Arusha, Liberatus Sabas amesema jeshi hilo limebaini vikundi vilivyojipanga kufanya vurugu na akavitaka kuacha kutekeleza mpango huo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda Sabas alisema wamebaini kuwa zaidi ya vijana 100 wamesambazwa mjini Arusha na Arumeru kwa ajili ya kufanya vurugu wakati wa uchaguzi.
Alisema polisi wamejipanga kukabiliana na uhalifu au vurugu zozote zitakazotokea katika kipindi cha uchaguzi kwa kuwa tayari wamepokea tetesi za kuwapo kwa makundi hayo.
“Natoa onyo kwa hayo makundi kuwa kama wanataka usalama waache mara moja kwa kuwa hawatakuwa salama,” alisema Liberatus.
Kamanda huyo aliwataka wakazi wa Arusha kupuuzia dhana potofu kuwa polisi wapo kwa ajili ya kupiga wananchi na kuwa, sheria itachukua mkondo wake kwa watakaofanya vurugu.
“Kazi ya polisi si kupiga watu ni kulinda. Sisi tunasema ukipiga kura na uende kwako kama sheria inavyosema, hakuna kukaa mita 200, 300 au 500, wote waende nyumbani,” alisema.
Alisema sheria inatambua wahusika wakuu wanaotakiwa kuwa vituoni, hivyo wasiotambuliwa na sheria ya uchaguzi waepuke mikusanyiko yoyote karibu na eneo la tukio.
“Hatutaki kuona mikusanyiko yoyote kwenye vituo vya kupigia kura. Ukikutwa mmoja au wawili au watatu tunahesabu kuwa ni mikusanyiko isiyo halali,” alisema Sabas.
Maoni
Chapisha Maoni