Maalim Seif: Msihofu..
Mgombea urais wa Zanzibar wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad akiwahutubia wananchi wakati akifunga kampeni za chama hicho katika Uwanja wa Maisara Unguja, jana.
Akihutubia maelfu ya wafuasi wa vyama vinavyounga Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wakati wa mkutano wa kuhitimisha kampeni zake kwenye Uwanja wa Mnazi Mmoja kisiwani Unguja, Maalim Seif aliwataka watumishi hao kuondoa hofu ya kufukuzwa kazi kwa kuipigia kura CUF.
“Hakuna kamera zitakazokuwa kwenye vyumba vya kupigia kura,” alisema Maalim Seif, ambaye kwa sasa ni Makamu wa Rais wa Zanzibar chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
“Kura utakayopiga ni siri yako na hakuna mtu yoyote atakayejua mgombea uliyempigia.”
Alisema kumekuwa na uzushi unaoenezwa na CCM kwamba watumishi wa Serikali, hasa askari wa KMKM, wametakiwa wasithubutu kuipigia CUF kwa kuwa watajulikana.
“Msiwe na wasiwasi, wanawatisha kwa sababu wanaona maji yamefika shingoni. Fanyeni uamuzi sahihi kwa kuichagua CUF ili iweze kuboresha maslahi yenu,” alisema.
Maalim Seif amemwomba Rais Jakaya Kikwete, ambaye ni amiri jeshi mkuu wa vikosi vya ulinzi na usalama kutofanya uamuzi utakaoitumbukiza nchi kwenye migogoro na vurugu.
“Rais wangu Kikwete, ninajua kuna wagombea unaowapenda na wengine usiowapenda. Wewe kama baba wa familia usibague, tenda haki ili kuepusha nchi isiingie kwenye vurugu.
“Ninawaelekeza wafuasi wa CUF kamwe wasifanye vurugu siku ya uchaguzi, lakini naomba Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) nayo itende haki.”
Katibu huyo mkuu wa CUF pia alimwomba Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kusimamia haki akisema uchaguzi isiwe sababu ya Wazanzibari kuuana.
“Dk Shein tuna uchaguzi keshokutwa. Elewa kwamba katika uchaguzi kuna uwezekano wa kushinda au kushindwa. Ukishindwa uwe imara kukubali matokeo, vinginevyo nchi ikichafuka wewe utakuwa mwajibikaji namba moja,” alisema.
“Mimi na wewe Dk Shein tuna jukumu kubwa la kuwaeleza wapigakura wetu kuwa katika uchaguzi kuna kushinda au kushindwa. Nikishindwa nitakuwa wa kwanza kukupongeza hadharani.”alisema
Hata hivyo, Maalim Seif alisema anamshangaa Dk Shein kutowajenga kisaikolojia wafuasi wake kwa kuwaeleza kuwa kushinda na kushindwa kunawezekana kwenye uchaguzi. Hata hivyo, mgombea huyo alisema kama Rais Kikwete na Shein watashindwa kusimamia haki katika uchaguzi huu, wasimtafute kama walivyokuwa wakifanya katika chaguzi zilizopita kwa kuwa hawatajua alipo.
“(Mwanasiasa mkongwe) Mzee Nassor Moyo, mambo yakiharibika wasije kukutuma kwangu kwa kuwa utanitafuta na hutaniona. Wenye kazi ya kudai Zanzibar yao ni vijana,” alisema.
Maalim Seif alilipongeza Jeshi la Polisi kwa kukiwezesha chama hicho kufanya mikutano yake kwa amani na utulivu tofauti na ilivyokuwa katika kampeni zilizopita.
“Polisi walituongoza vizuri kwenye mikutano yetu ya kampeni kulikuwa na amani na utulivu. Tunaomba hayo yaendelee siku ya uchaguzi,”alisema.
Kwa upande wake, mgombea mwenza wa urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chadema, Juma Duni Haji alisema kwa mara ya kwanza wamepata mgombea wa urais wa Tanzania ambaye amekubali kushirikiana na Zanzibar ili kupata serikali tatu.
“Wenzenu Tanzania Bara wako tayari kwa mabadiliko na nyie mko tayari?” aliuliza na kujibiwa, “tuko tayari”.
Akihutubia kwenye mkutano huo, Moyo alisema wakati walipoteuliwa, viongozi wa ZEC walikula kiapo kwa kushika kitabu cha Quran kueleza kuwa watatenda haki.
Maoni
Chapisha Maoni