Wasanii hawa wamepeta Uchaguzi Mkuu 2015..
Miezi michache baadaye waliogombea wakajulikana na wengine wakibaki kuwa wasindikizaji ambao walijiunga sambamba na wale walioshinda katika viti mbalimbali kwa ajili ya kuwapigia debe.
Awali makundi mbalimbali ya kijamii yalijitokeza kutangaza nia na kundi lililotia fora zaidi lilikuwa ni la wasanii walioonyesha nia ya kuwatumikia wananchi katika nyadhifa mbalimbali ikiwamo ubunge na udiwani.
Zaidi ya wasanii 50 walitangaza nia katika nyadhifa hizo, licha ya wachache kufikia katika hatua ya kupigiwa kura na wananchi na walichujwa Oktoba 25 na wachache kati yao kuibuka vinara.
Frank Mohamed Mwikongi aliwania ubunge kupitia ACT Wazalendo Jimbo la Segerea, Selemani Msindi ‘Afande Sele’ aligombea kupitia ACT Jimbo la Morogoro Mjini, Karama Masoud ‘Kalapina’ aligombea Jimbo la Kinondoni ACT.
Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ Jimbo la Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Haule ‘Profesa Jay’ jimbo la Mikumi (Chadema) na Rashid Mwinshehe ‘Kingwendu’ Jimbo la Kisarawe kupitia CUF.
Kati ya hawa walioibuka kidedea ni pamoja na Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ alishinda kwa mara nyingine kiti cha ubunge alichokuwa akitetea tangu mwaka 2010.
Kwa mara nyingine wananchi wa jimbo lake, wamempa ridhaa ya kuwaongoza kwa kipindi kingine.
Profesa Jay anakuwa msanii wa pili Tanzania kuwahi kushikilia kiti cha ubunge baada ya kutangazwa mapema wiki hii kuwa ndiye mshindi wa Jimbo la Mikumi katika uchaguzi huo baada ya kupata kura 32,259.
Profesa Jay ambaye alikuwa akiwania kiti hicho kwa tiketi ya Chadema alimshinda mpinzani wake wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Jonas Nkya ambaye alipata kura 30,425.
Meneja wa Kituo cha Mkubwa na Wanawe ambaye pia ni meneja wa TMK Wanaume Family Said Hassan, maarufu Mkubwa Fela aliwania udiwani na alipata kura 7,843, dhidi ya mpinzani wake Suday Emanuel aliyepata kura 4,045.
Fella anakuwa diwani wa Kata ya Kilungule iliyopo katika Jimbo la Mbagala kwa mara ya kwanza tangu aliposhikilia nyadhifa mbalimbali za uongozi wa chini ndani ya chama chake.
“Kata yangu ilikuwa na vituo vingi, kura zilipigwa vizuri na kwa utulivu na katika kata yangu wananchi walinihitaji kwani hakuna madhara yoyote yaliyotokea baada ya uchaguzi hata malalamiko, hivyo mimi ni mmoja kati ya madiwani 10 wa Jimbo la Mbagala,” alisema Fella.
Clayton Revocatus Chiponda ‘Baba Levo’ yeye ameshinda kiti cha udiwani katika Kata ya Mwanga mkoani Kigoma, alisema aligombea katika kata hiyo kwa kuwa aliona na kuamini kwamba yeye ndiye anayeweza kuwazungumzia na kuwatetea wananchi wa kata hiyo.
Clayton alishinda kiti cha udiwani kupitia ACT baada ya kupata kura 2997 dhidi ya mpinzani wake Omary Sebabili wa CCM aliyepata kura 2,764, huku mpinzani mwingine kutoka Chadema, Francis Mangu akipata kura 2,040. “Nimeshinda katika vituo 25 kati ya vituo 31 ambavyo vilipigiwa kura katika kata niliyogombea, nashukuru Mungu nimeshinda kwani wananchi walijua fika kwamba nilikuwa na nia ya dhati ya kuwasaidia katika kata yangu, naomba Mungu anipe uzima ili nifanikishe malengo niliyoyakusudia katika kata yangu,” alisema Baba Levo.
Kwa Profesa Jay ilikuwa ni ndoto ya muda mrefu. Mei 2013 Profesa Jay alijiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na katika mahojiano na gazeti hili aliweka wazi kwamba hakuingia ili kugombea ubunge, bali lengo lake lilikuwa kuongeza nguvu katika chama hicho ambacho aliamini kwamba kina sera sahihi kwake na uwezo wa kuikomboa nchi.
Lakini baadaye mawazo yake yakabadilika baada ya kukaa katika chama kwa miaka miwili, mwaka jana Profesa Jay aliliambia Mwananchi nia yake ya kuja kushiriki siasa japo hakuifafanua kwa undani zaidi.
Profesa Jay alisema kwa muda mrefu amekuwa akibuni na kuimba mashairi ya masuala ya kisiasa tangu anaanza muziki mwanzoni mwa miaka ya 1990, hivyo ana dhamira ya kuja kuwasaidia Watanzania kwa vitendo.
Kauli hiyo imejidhihirisha sasa, baada ya rapa huyo kuchaguliwa kuwa mmoja kati ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiliwakilisha jimbo la Mikumi.
Kauli ya Profesa Jay
Siku moja baada ya kutawazwa rasmi kuwa Mbunge wa Jimbo la Mikumi, Profesa Jay amefanya mahojiano na gazeti hili na kueleza siri ya mafanikio yake na namna alivyofanya kampeni ya nyumba kwa nyumba.
Profesa Jay anasema licha ya kwamba alikuwa katika chama pinzani, aliwaambia wazi wananchi wa Mikumi matarajio yake akiwa mbunge na nini atafanya iwapo atachaguliwa kuwa mbunge wao ikiwa ni pamoja na kutoweka itikadi za vyama kwani lengo kubwa ni kuipigania Mikumi.
“Nilizungumza nao sikupenda makundi, sikujali ni CCM au chama chochote kingine, ndoto zangu ni kuwafanya wananchi wa Mikumi wawe wamoja wenye kusaidiana na kupeleka mbele gurudumu la maendeleo, nimezaliwa huko na familia yangu ipo huko, nina uchungu na jimbo langu najua nina mengi nitayafanya kwa kipindi hiki cha miaka mitano,” anasema Profesa Jay.
Muziki je?
Kama kuna kitu ambacho Profesa Jay atahisi kudhulumiwa, basi ni kuacha muziki. Kwa mujibu wa rapa huyu anasema atafanya shughuli zote za Bunge na hata kazi za kuwahudumia wananchi wake, lakini kazi yake ya muziki ni kipaji hivyo hawezi kuacha.
Anasema anachoweza kufanya sasa ni kuwasaidia wasanii wenzake kuwasemea na kutafuta njia za kuwakomboa, lakini kubwa kwake ni kusaidia vijana wa Tanzania kwa mambo mbalimbali.
“Wapo wachungaji ambao waliingia katika siasa hawakuacha kuhubiri, wapo wafanyabiashara ambao nao waliingia huko hata nao hawakuacha biashara zao.
Kwa upande wangu siwezi kuacha, nitaendelea kufanya muziki mpaka mwisho wa maisha yangu,” anasema Profesa Jay.
Maoni
Chapisha Maoni