Wagombea CCM, Ukawa vinara wa kutoa rushwa..
Mwenyekiti mwenza wa Cemot, Dk Benson Bana.
Dar es Salaam. Mwamvuli wa waangalizi wa ndani wa uchaguzi (Cemot), umetoa ripoti ya mwenendo wa kampeni za Uchaguzi Mkuu nchini wa mwezi mmoja inayoonyesha kuwa CCM imeongoza kwa kujihusisha na rushwa ikifuatiwa na Ukawa.
Mwenyekiti mwenza wa Cemot, Dk Benson Bana aliwaambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuwa, kati ya waangalizi 301 waliowapatia taarifa za uangalizi, asilimia 29 walisema wamesikia wawakilishi wa CCM wakijihusisha na vitendo vya rushwa wakati wa Ukawa ni asilimia tisa.
Hata hivyo, Msemaji wa Kamati ya Kampeni ya CCM, January Makamba alipoulizwa kuhusiana na utafiti huo, alisema hauna ukweli wowote na kudai kuwa wamekuwa wakiwasisitiza na kuwafuatilia wagombea wao ili kujiepusha na vitendo hivyo.
Hivyo, alisema wana uhakika wagombea wao wanazingatia Sheria ya Uchaguzi na ile ya Gharama za Uchaguzi.
“Tumesikitishwa na taarifa hiyo maana kama ina ukweli basi wangeeleza na kutaja matukio hayo badala ya kuzungumza kwa ujumla,” alisema Makamba.
Naye Msemaji wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Tumaini Makene aliukosoa utafiti huo akisema hakuna chama kinachoitwa Ukawa. Aliwataka watafiti hao kuwa makini wanapotoa taarifa za namna hiyo kwa jamii kwa kuchanganua wanachotaka kukisema ili waeleweke.
Dk Bana alisema waangalizi hao walitoa taarifa kuwa hawakusikia vitendo vya rushwa kwa kiwango kikubwa katika vyama vingine vya siasa vilivyosimamisha wagombea.
Cemot ni muungano wa Taasisi ya Waangalizi wa Uchaguzi wa Ndani (Temco) na umoja wa waangalizi wa uchaguzi kutoka asasi za kiraia Tanzania (Tacceo).
Kwa pamoja wanafuatilia mwenendo wa Uchaguzi Mkuu utakaofanyika keshokutwa.
Dk Bana alisema taarifa hizo walizikusanya kati ya Septemba 25 na Oktoba 21, kutoka kwa waangalizi 301 kati ya 350, ambao wanatoa taarifa za mwenendo wa uchaguzi kwa kupitia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), kwenye majimbo 229 ya uchaguzi.
Alisema waangalizi hao pia ni sehemu ya waangalizi 8,450 waliopelekwa katika majimbo yote 265 nchini.
“Asilimia 30 ya waangalizi wetu wamesikia kuwapo kwa vitendo vya kusafirisha wapigakura kwenda kushiriki mikutano ya hadhara kwa CCM,” alisema .
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa Ukawa wanafuatia kwa kusafirisha wapigakura kwenda kwenye mikutano ya kampeni kwa asilimia 12, wakati asilimia tano ni kwa vyama vingine.
Dk Bana alisema nusu ya mikutano ya kampeni iliyoshuhudiwa ni ya ubunge katika majimbo yote nchini.
Maoni
Chapisha Maoni