TCRA yasisitiza amani ya nchi ilindwe..
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui ya TCRA, Magreth Munyagi alisema vyombo vya utangazaji vinapaswa kukumbuka kuwa mshikamano, umoja na amani ni tunu muhimu ya Taifa ambayo inapaswa kulindwa na kudumishwa.
Alisema mamlaka hiyo inaendelea kufuatilia vipindi vyote vya uchaguzi ili kuhakikisha kuwa havikiuki sheria na kanuni za nchi.
Munyagi alivitaka vyombo vya utangazaji kutangaza habari zinazotokana na vyanzo vinavyoaminika, na endapo chombo chochote kitakiuka agizo hilo kitaadhibiwa kwa kupewa onyo, kupigwa faini, kufungiwa kurusha matangazo kwa muda au kunyang’anywa leseni.
Pia alivikumbusha vyombo vyote hivyo kuzingatia kanuni zinazoongoza namna ya kusimamia na kutangaza midahalo ya kisiasa endapo ipo inayotarajiwa kufanyika katika kipindi cha siku chache zilizosalia kabla ya uchaguzi.
Mwenyekiti huyo alivipongeza vituo vya utangazaji kutimiza kwa wastani wajibu wa kisheria, kwa kutangaza vipindi vinavyolinda na kutetea amani sambamba na kuepuka uchochezi.
Alisema katika kipindi cha wiki mbili zilizopita kumekuwa na maboresho ya kuridhisha kwenye vipindi vinavyorushwa, huku kukiwa na mizania inayozingatiwa katika kutangaza kampeni za vyama vyote vya siasa.
“Navipongeza vyombo vyote vya utangazaji, jitahidini kuhakikisha kuwa vipindi vyote vya redio na televisheni vikiwamo vile vya mahojiano, vya ushirikishwaji wa wananchi kwa njia ya simu na vingine vya moja kwa moja vinazingatia maadili,” alisema.
Maoni
Chapisha Maoni