Watu 27 wafariki katika mkasa moto wa Romania..
Rais wa Romania Klaus Iohannis amesema amehuzunishwa sana na mkasa huo.
Watu 27, wengi wao vijana wadogo, wamefariki baada ya moto kuzuka katika kilabu kimoja cha usiku mjini Bucharest, Romania.
Moto huo ulitokea katika kilabu cha Colectiv Ijumaa usiku na kusababisha mkanyagano watu wakikimbilia milango kujiokoa.
Afisa mkuu wa huduma za dharura Raed Arafat amesema watu 155 wanatibiwa katika hospitali mbalimbali katika jiji hilo kuu la Romania.
Moto huo unaaminika kuwa ulianzishwa na fataki ambazo ziliwashwa ndani ya kilabu.
"Habari tulizo nazo ni kwamba kulikuwa na fataki zilizowashwa kwenye kilabu hiki na baada ya hapo mkasa ulitokea. Bila shaka, kisa hiki kinachunguzwa,” Bw Arafat ameambia BBC.
Fataki zilikuwa zinatumiwa na bendi iliyokuwa ikitumbuiza. Mmoja wa walioshuhudia anasema kulitokea cheche ambazo zilifanya fataki kushika moto. Muda mfupi baadaye moja ya nguzo za nyumba ilishika moto na mwishowe moto ukafikia dari na mlipuko mkubwa ukatokea.
"Watu walikuwa wakizirai, walikuwa wanazirai kutokana na moshi. Ilikuwa na vurugu, kila mtu akikimbia kujaribu kujiokoa,” Victor Ionescu, aliyekuwa kwenye kilabu hicho, ameambia kituo cha habari cha Romania kwa jina Antena 3.
Inakadiriwa watu 400 walikuwepo kwenye kilabu hicho wakati wa kutokea kwa janga hilo.
25 kati ya majeruhi wamo katika hali mahututi
Waziri Mkuu Victor Ponta amesema atasitisha ziara yake nchini Mexico na kurejea Bucharest.
Rais wa Romania Klaus Iohannis ameandika kwenye ukurasa wake wa Facebook kwamba amehuzunishwa sana na mkasa huo.
“Ni siku ya huzuni kubwa sana kwetu sote, kwa taifa letu na kwangu binafsi.”
SOURCE:BBC
Maoni
Chapisha Maoni