Mawaziri waanguka...
MAWAZIRI mbalimbali waliokuwa wanatetea nafasi zao za ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameangushwa katika kinyang’anyiro hicho.
Walioangushwa ni pamoja na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira aliyekuwa akitetea Jimbo la Bunda Mjini. Wasira ameangushwa na Esther Bulaya wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Wengine ni Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Kebwe Steven Kebwe (Serengeti) aliyeangushwa na Marwa Chacha Ryoba wa Chadema na Naibu Waziri wa Tamisemi, Aggrey Mwanri aliyekuwa Mbunge wa Siha ambaye ameshindwa na Godwin Mollel wa Chadema.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uwekezaji na Uwezeshaji), Christopher Chiza, aliyekuwa akitetea Jimbo la Buyungu mkoani Kigoma, ameangushwa na Bilago Samson wa Chadema.
Mwingine aliyeangushwa ni Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Anna Kilango, aliyekuwa akitetea ubunge wake katika Jimbo la Same Mashariki.
Katika jimbo hilo, mgombea wa Chadema, Naghenjwa Kaboyoka, ndiye aliyeibuka mshindi kwa kupata kura 18,839 dhidi ya kura 15,539 alizopata Kilango.
WASHINDI MAJIMBO MENGINE
Wakati huohuo, hadi jana CCM ilikuwa inaongoza kwa kupata viti vingi vya wabunge ikifuatiwa na Chadema na Chama cha Wananchi (CUF).
Wagombea wengine waliotangazwa kushinda kwa upande wa Tanzania Bara kwa vyama vyote ni Antony Mavunde (CCM) Dodoma Mjini, Suleman Jafo (CCM) Kisarawe, Cosato Chumi (CCM) Mafinga, Ridhiwani Kikwete (CCM) Chalinze, Syven Koka (CCM) Kibaha Mjini na Janeth Mbene (CCM) Ileje.
Wengine ni David Mathayo (CCM) Musoma Mjini, Shukuru Kawambwa (CCM) Bagamoyo Mjini, Chacha Ryoba (Chadema) Serengeti na Angelina Mabula (CCM) aliyeshinda katika Jimbo la Ilemela.
Wengine ni Rashid Abdallah (CUF) Mtwara Mjini, Sixtus Mapunda (CCM) Mbinga Mjini, Mwigulu Nchemba (CCM) Iramba Mashariki na Steven Masele (CCM) Shinyanga Mjini.
Washindi wengine ni Freeman Mbowe (Chadema) Jimbo la Hai, Julius Kalanga (Chadema), Mwakajoka Frank (Chadema) Tunduma, Bilago Samson (Chadema) Buyungu, Ester Matiko(Chadema) Tarime Mjini, Hassan Kaunje (CCM) Lindi Mjini na Ahmed Katani (CUF) Tandaimba.
MbingaVijijini aliyeshinda ni Martin Msuha (CCM) huku Mbeya Mjini akishinda Joseph Mbilinyi (Chadema), Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Mzalendo) na Daniel Nsanzugwanko (CCM) aliyemuangusha Moses Machali wa ACT-Wazalendo katika Jimbo la Kasulu.
KONGWA
Katika Jimbo la Kongwa aliyekuwa Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai (CCM), aliibuka kidedea kwa kupata kura 73,165 sawa na asilimia 76.89 akimshinda mpinzani wake Ngobei Fremont aliyepata kura 20,335 sawa na asilimia 21.37. Katika jimbo hilo, kata zote 22 zimechukuliwa na CCM.
MPWAPWA
Jimbo la Mpwapwa, George Lubeleje (CCM), aliibuka mshindi kwa kupata kura 32,208 sawa na asilimia 74.46 akimshinda mpinzani wake Ezekiel Chisinjila wa Chadema aliyepata kura 11,048 sawa na asilimia 25.04. Matokeo hayo ni kwa mujibu wa Msimamizi wa Uchaguzi, Mohammed Maje ambaye alisema kata zote 15 zilichukuliwa na CCM.
TARIME VIJIJINI
Katika Jimbo la Tarime Vijijini, mgombea wa Chadema, John Heche ameibuka mshindi baada ya kupata kura 47,249 akifuatiwa na Christopher Kangoye wa CCM kura 42,325, Charles Mwera wa ACT (1,846) na Chingwa Migera wa Chausta kura 365.
SIMIYU
Mkoani Simiyu, CCM imetangazwa kushinda Maswa Mashariki ambako Stanslaus Nyongo amemshinda Slivester Kasulumbayi (Chadema) wakati Maswa Magharibi, Ndaki Mashimba wa CCM amemshinda John Shibuda (ADA TADEA) huku katika Jimbo la Meatu, Salum Hamis wa CCM naye akimshinda Meshark Opulukwa wa Chadema.
ILEMELA
Katika Jimbo la Ilemela aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo kwa tiketi ya Chadema, Haines Kiwia amepoteza ubunge.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela, John Wanga alisema Angelina Mabula (CCM) ameshinda kwa kupata kura 85,424 huku Kiwia akipata kura 61,679.
CUF YASHINDA MTWARA MJINI
Chama cha Wananchi (CUF) kimechukua Jimbo la Mtwara Mjini kwa kishindo baada ya mgombea wa CCM, Hasnain Murji kushindwa kutetea kiti chake.
Msimamizi wa uchaguzi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani, Limbakisye Shimwela alisema Maftaa Nachuma wa CUF alishinda kwa kupata kura 26,655 wakati Murji wa alipata kura 24,176.
Naye Msimamizi wa wa Uchaguzi wa Jimbo la Mtwara Vijijini ambaye pia ni Mkurugezni wa Halmashauri ya Mtwara Vijijini, Zakaria Nachoa alisema Hawa Ghasia wa CCM ametetea kiti chake kwa kupata kura 24,258.
Alisema kati ya kata 21 zilizopo wilayani hapo, 13 zimechukuliwa na CCM, na CUF saba.
Mwalongo amrithi Makinda
Msimamisi wa uchaguzi katika jimbo la Njombe Kusini, Elminata Mwenda ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe, jana alimtangaza Edward Mwalongo kuwa mbunge wa Njombe Kusini baada ya kupata kura 27,285 na kumshinda Emaanuel Masonga wa Chadema aliyepata kura 23,003.
Mwenda alisema mgombea wa ACT, Emilian Msigwa alipata kura 3,888 wakati mgombea wa DP, William Myegeta alipata kura 94.
Akizungumza baada ya kutangazwa kuwa mshindi, Mwalongo aliahidi kushirikiana na wananchi katika kuleta maendeleo, hususan kutatua kero ya maji ambayo imekuwa ikilalamikiwa na wananchi mjini Njombe.
“Naomba sana wana Njombe tushikamane, tufanye kazi, kwa sababu kaulimbiu yetu hivi sasa ni Hapa Kazi Tu, changamoto zilizopo Njombe Kusini utatuzi wake kwanza kabisa ni mshikamano wa wana CCM wenyewe.
“Kwa kweli najisikia faraja kulitumikia jimbo lililokuwa likiongozwa na Spika Anne Makinda, naona nina wajibu mzito ambao natakiwa kulitumikia Jimbo la Njombe Kusini, mama yule alikuwa ni mahiri katika siasa na vilevile katika uongozi,” alisema.
Katika jimbo hilo kata nane zimechukuliwa na CCM, na kata tano zimekwenda kwa Chadema.
CUF YASHINDA MARA YA KWANZA TANGA
Mgombea ubunge Jimbo la Tanga kupitia CUF, Mussa Mbaruku, ameibuka kidedea katika kinyang’anyiro cha ubunge wa jimbo hilo baada ya kuwabwaga wapinzani wake.
Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Tanga, Daudi Mayeji alisema Mbaruku alipata kura 58,665 huku anayemfuatia, Omari Nundu wa CCM akipata kura 57,114 .
Aliwataja wagombea wengine na kura walizopata kuwa ni Kidege Hamad Mohamed (ACT) aliyepata kura 1,832 na Jaribu Ally wa ADC akipata kura 1,144 na Mwamvita Mashaka wa Chauma kura 197.
Akizungumza baada ya kuibuka mshindi kwenye uchaguzi huo, Mbaruku alisema mipango yake mikubwa ni kuhakikisha anaibadilishaTanga kuwa ya viwanda ili kuweza kukuza uchumi wa mkoa huu.Alisema kuwa uchumi wa mkoa ulikuwa umedodora kutokana na kutokuwapo viwanda ambazo zilikuwepo vinafanya kazi katika miaka iliyopita na kuufanya mkoa huu kuwika na kuweza kuchangia pato la mkoa na taifa kwa ujumla.
“Niwashukuru wapiga kura wangu lakini kubwa niwaahaidi wananchi wa Jimbo la Tanga nitahakikisha nachangia maendeleo ya mkoa wa Tanga kwa vitendo wananchi waweze kupata mafanikio.
Wakati huohuo, Jeshi la Polisi mkoani Tanga lililazimika kulipua mabomu kutawanya wananchi waliokuwa wamekusanyika nje ya ofisi za Halmshauri ya Jiji la Tanga baada ya matokeo kutangazwa.
Wafuasi wa mgombea ubunge huyo waliokuwa wamefurika nje ya jengo hilo waligoma kutawanyika eneo hilo ndipo jeshi hilo lilipofaetua mabomu hayo. Wananchi hao walikuwa wakishangilia ushindi wa mbunge huyo ambaye ameweka historia ya kuliongoza akiwa upande na upinzani tangu lilipoanzishwa.
SOURCE:Mtanzania
Maoni
Chapisha Maoni