Wanasheria wataka Jecha achunguzwe..
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Salim Jecha Salum.
Zanzibar: Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS) kimetaka iundwe tume huru ya kuchunguza jinsi mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Salim Jecha Salum alivyofikia uamuzi wa kufuta matokeo na akithibitika kuwa alishinikizwa, afukuzwe kazi.
Wakati wanasheria wakitoa pendekezo hilo, mmoja wa wagombea urais wa Zanzibar, Hamad Rashid Mohamed wa chama cha ADC, amesema hana imani na ZEC na kuwataka wajumbe wawajibike kwa kujiuzulu.
Katibu wa ZLS, Omar Said Shaaban ambaye alikuwa ameambaatana na rais wake, Wakili Awadh Ali Said, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa tamko la Jecha la kufuta matokeo ya uchaguzi halina nguvu na linaweza kuhatarisha amani.
“Rais aone haja ya kuunda Tume ya kumchunguza mwenyekiti dhidi ya madai ya kushindwa kufanya kazi zake na ikiwa madai hayo yakithibitika, basi amuondoe mara moja,” alisema Shaaban kwenye mkutano huo uliofanyika ukumbi wa Ulemavu, Kikwajuni.
Oktoba 28, Jecha alisema kwenye mkutano na waandishi wa habari wa vyombo vya Serikali kuwa amefuta matokeo yote ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofanyika Oktoba 25 baada ya kujhiridhisha kuwa kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa sheria na taratibu na kwamba mmoja wa wagombea urais alishajitangazia matokeo yanayompa ushindi.
Lakini wanasheria hao wametaka uchaguzi huo uendelee kuanzia pale ilipoishia, yaani hatua ya kufanya majumuisho ya kura za urais ili mshindi halali wa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofanyika tarehe 25 Oktoba, 2015 apatikane na kutangazwa kuwa Rais.
Chama hicho kimevitaka vyombo vya dola kuchunguza na kuwakamata na hatimaye kuwafikisha mahakamani watu wote waliohusika kumshinikiza mwenyekiti kutoa tamko la kufuta uchaguzi na matokeo yake.
Mbali ya hayo, chama hicho kimetoa wito kwa viongozi wote wa vyama vya siasa kujitathmini wajibu wao katika kuheshimu maamuzi ya wananchi yanayofanywa kwa njia ya demokrasia ili kujenga misingi mizuri ya utawala bora.
“Tunaamini kwamba Rais wetu wa Zanzibar atang’amua mtego huu unaokusudia kumuweka katika Historia ya Rais wa Zanzibar aliewahi kuvunja Katiba ya Nchi na kumuondolea rekodi nzuri aliyonayo ya kuheshimu sheria na Katiba ya Nchi na Utawala Bora” alisema Shaaban.
Kwa upande wake Rais wa chama hicho Awadh Ali Said alisema Chama Cha Wanasheria Zanzibar kimefadhaishwa na uamuzi huo hasa kwa kuzingatia mamlaka aliyonayo Mwenyekiti huyo kisheria katika kufikia Uamuzi kama huo.
Alisema Chama cha Wanasheria kimepitia kwa umakini Katiba ya Zanzibar ya 1984 na Sheria ya Uchaguzi Nambari 11 ya 1984 ili kujiridhisha kama Mwenyekiti anao uwezo wa Kufuta matokeo ya Uchaguzi kama alivyoeleza kwenye tamko lake na kama sababu zilizoelezwa zinakidhi kufutwakwa Uchaguzi Nchi nzima.
Akitaja vifungu vya sheria, rais huyo alisema kwa mujibu wa Ibara ya 119 (1) ya katiba ya Zanzibar ya 1984, tume ni mwenyekiti pamoja na Wajumbe wengine Sita kama walivyoanishwa na ibara hiyo na kwamba maamuzi yoyote ya Tume, lazima yaungwe mkono na wajumbe walio wengi.
Alisema licha ya utashi huo wa kisheria, wajumbe wawili walitoka hadharani mbele ya waandishi na kusema hawajashirikishwa.
“Taarifa iliyotolewa kwa waandishi na wajumbe wa Tume, Nassor Khamis na Ayoub Bakari, kuwa hakukuwa na kikao chochote kilichofikia uamuzi wa kufuta Uchaguzi wa Zanzibar, haijapingwa mpaka sasa na wajumbe wengine wa Tume. Hii inaleta taswira ya wazi kuwa uamuzi huo haukuwa wa Tume, bali ni wa mtu mmoja ambaye ni mwenyekiti, hivyo kuyafanya kuwa ni batili mbele ya macho ya Sheria,” alisema Said.
Pia walisema kanuni ya 41(1) imeweka wazi utaratibu kufutwa kwa siku ya uchaguzi na kutangazwa siku nyengine na namna uamuzi huo utakavyofikiwa na sio kufuta matokeo ya Uchaguzi au Uchaguzi wenyewe.
“Ni kwa bahati mbaya sana Mwenyekiti katika Tamko lake hakueleza kama utaratibu umefatwa. Huu ni ukiukwaji mkubwa wa Sheria” aliongeza Rais wa chama hicho.
“Kwa Mujibu wa Sheria, Tume haina uwezo wala Mamlaka ya kufuta matokeo yaliyotangazwa na taayari mgombea ameshapewa shahada ya kuchaguliwa”.
Rais huyo alisema wajibu wa Tume ni kuchapisha matokeo hayo kwenye gazeti la serikali kama kanuni ya 59 (4) na kifungu cha 88 (c) cha Sheria ya Uchaguzi vinavyoeleza na kama kuna Mgombea ambae hajaridhika na matokeo au maamuzi ya Msimamizi wa Uchaguzi basi anatakiwa kwenda Mahakama Kuu kwa mujibu wa kifungu cha 86 cha Sheria ya Uchaguzi na Ibara ya 72 (1) ya Katiba ya Zanzibar ya 1984 ambayo ndio yenye mamlaka ya kufuta uchaguzi na matokeo yake.
Akizungumzia athari za tamko la mwenyekiti huyo wa ZEC, alisema linaweza kuiingiza nchi katika mgogoro mkubwa wa kikatiba kama kumalizika kwa muda wa mwisho wa utawala wa serikali ya sasa kwa mujibu wa ibara ya 28 (2) ya Katiba ya Zanzibar ya 1984. Ibara hiyo inaeleza kuwa rais ataacha madaraka yake baada ya kumalizika miaka mitano kuanzia tarehe alipokula kiapo.
Alisema Rais Mohamed Shein alikula kiapo cha uaminifu na Novemba 3, 2010 na hivyo atamaliza muda wake Novemba 3.
“Hivyo akiendelea kushikilia urais zaidi ya tarehe hiyo, itakuwa kinyume na katiba ya nchi. Upo mjadala katika jamii kuwa Rais anao uhalali wa kuendelea kuwa Rais chini ya Ibara ya 28 (1) (a). Maoni ya Chama cha Wanasheria Zanzibar ni kuwa maudhui ya Ibara hiyo ni kumpa uwezo wa kikatiba Rais kuendelea ili kutoa nafasi ya maandalizi ya kula kiapo kwa Rais mpya tu na sio kuendelea kukaa madarakani bila ya kufanyika kwa uchaguzi au kwa sababu ya kufutwa kwa uchaguzi,” alisema Said.
Pia alisema katika mazingira yaliyopo nchi itaendeshwa kwa muda mrefu bila ya kuwepo kwa Baraza la Wawakilishi ambalo ni mhimili muhimu katika uendeshaji wa Serikali.
Alisema katiba ya Zanzibar imeruhusu nchi kuendeshwa bila ya baraza hilo kwa siku 90 tu kuanzia siku Baraza lilipovunjwa.
“Kwa mazingira tuliyonayo, siku tisini zinazokubalika kikatiba zinaishia Novemba 12, 2015 kwa kuwa Baraza la Wawakilishi lilivunjwa tarehe Agosti 13, 2015,” alisema.
Pia alieleza utata wa kisheria uliopo kwa mujibu wa ibara ya 37 ya katiba ya Zanzibar ambayo inaipa mamlaka Baraza la Wawakilishi kuondoa kinga ya Rais kutoshtakiwa anapokuwa madarakani kama inavyotolewa na Ibara ya 36 ya Katiba.
Alisema katika mazingira yaliyopo hivi sasa, ifikapo Novemba 12, Baraza la Wawakilishi halitakuwepo na haliwezi kuitishwa kikatiba, ni wazi kuwa ikiwa Rais atafanya matendo yoyote yenye kuvunja katiba ya nchi na kukiuka kiapo chake, hakutakuwa na mamlaka nyingine yenye uwezo wa kuhoji vitendo vya Rais.
Katika hatua nyingine, Hamad Rashid amewaambia waandishi wa habari jana kuwa kwenye ukumbi wa Hoteli ya Grand Malt, Malindi kuwa chama chake kimekosa imani na ZEC kutokana na uendeshaji wake kukosa sifa ya kufuata sheria na kanuni.
Alisema kuwa ili uwazi na uwajibikaji viweze kufikiwa, hakuna budi kwa watendaji wa tume huyo kujiuzulu na badala yake iundwe Tume yenye uwakilishi mpana na usio na mrengo wa kisiasa.
Alisema kuwa hatua hiyo kwa kiasi kikubwa inaweza kufanikisha kufanyika kwa uchaguzi wa amani na utulivu huku democrasia ikichukua mkondo wake.
Maoni
Chapisha Maoni