Moyo:Mambo saba yataiponza CCM..



Mzee Hassan Nassoro MoyoMzee Hassan Nassoro Moyo.
Mwishoni mwa wiki iliyopita nilikwenda Zanzibar. Nilishangaa kuona utitiri wa picha za mgombea urais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kwenye kuta za majengo yaliyo karibu na bandari.
Kilichonishangaza ni maandishi yasemayo; “Chagua CCM, Chagua Shein: Umoja ni Ushindi” wakati picha chache za mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano zimeandikwa: “Chagua Magufuli” huku zikiwa na nembo ya CCM.
Eneo la Darajani kuna picha chache za mgombea wa CUF, Seif Sharrif Hamad, lakini kuna bendera nyingi za Ukawa huku Kisiwandui zikitawala bendera za CCM hadi Fuoni. Dereva teksi aliniambia, “Ungekuja wiki iliyopita ungekuta picha nyingi za wagombea wetu. Wamezitoa wakabandika zao.   
Maalim Seif ametuambia tusigombane kwa sababu ya picha na vitambaa (bendera).”
Fuoni ni kwa mwenyeji wangu, Hassan Nassor Moyo (80) mwanasiasa mkongwe na kada wa zamani wa CCM. Tangu avuliwe uanachama Aprili mwaka huu, amekuwa akifuatilia mwelekeo wa siasa na hasa kampeni za uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 kwa jicho huru.
Tathmini
Akijibu swali, katika tathmini yake ni chama gani anakipa nafasi ya kushinda katika Uchaguzi Mkuu, kwanza alikiri kwamba kampeni ni kali na mchuano ni mkali Zanzibar kati ya CCM na CUF ilhali Tanzania Bara ni kati ya CCM na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
“Labda niseme tu nchi mbili hizi (Zanzibar na Tanzania Bara) zina historia ndefu. Wakati zinapata uhuru kulikuwa na vyama vingi, baadaye ilitungwa sheria kuwa na mfumo wa chama kimoja; Zanzibar ilibaki na ASP na Bara ilibaki Tanu, mwaka 1977 vyama hivyo vikaunganishwa ndipo ikazaliwa CCM lakini mwaka 1992 ulirejeshwa mfumo wa vyama vingi,” anasema Moyo.
“…Baada ya mapinduzi iliundwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar iliyoshirikisha viongozi wa vyama vya Hizbu, Umma Party, na ASP. Serikali ilichanganya viongozi wa vyama vyote, sheria ilitungwa kuondoa ubaguzi, uongozi ulikuwa wa pamoja. Huo ndiyo ulikuwa msingi wa hata Rais Amani Karume na Seif Sharrif Hamad kufanya maridhiano,” anasema.
“Leo kila mmoja anajiona hodari, wengine wanajiona wamedharauliwa. Tunagombana kwa sababu ya vyama vingi. Mpinzani tunamuona adui jambo ambalo ni kosa. CCM ndio walikubali Katiba ikabadilishwa lakini leo wanamwona Maalim Seif ni adui yao, hili ni kosa kubwa kwani limekijengea chama mazingira magumu.”
Kosa la pili alilolibaini ambalo anasema linaiweka CCM katika wakati mgumu ni lile lililofanywa wakati wa kuteua mgombea urais. Hapo aliungana na Kingunge Ngombale-Mwiru (aliyejiondoa CCM) kusema kulikuwa na ukiukwaji wa kanuni wakati wa kuteua mgombea urais.
Kwamba Kamati Kuu ilipaswa kuwajadili wagombea wote na kupitisha majina matano ili yakajadiliwe katika Halmashauri Kuu ya Taifa ambayo pia ingepeleka majina matatu kwenye mkutano mkuu kupata jina moja lakini haikuwa hivyo hali iliyosababisha mpasuko ndani ya chama.
“Mwalimu Julius Nyerere aliposema upinzani wa kweli utatoka ndani ya CCM, ni kwa vitendo vyetu. Viongozi wetu walikuwa na watu mfukoni, wakaona wamchukue yeyote barabarani. Unawezaje kumteua mtu ambaye hajawahi hata kuwa balozi wa nyumba 10? Je, anaijua misingi ya chama? Anakijua chama? Anatosheleza?” anahoji.
“Mgombea wa CCM, John Magufuli ilikuwa ajadiliwe na Kamati Kuu kama zinavyosema kanuni lakini haikufanyika. CCM tuna tabia ya kumfuata kiongozi hata anapokosea utaona wananong’ona pembeni ‘mkubwa anataka.’ Kwa hali hii upinzani umepewa nafasi ya kushinda na dalili zinaonekana,” anasema.
Moyo anasema madhara ya ukiukwaji wa taratibu za kumpata mgombea urais, baadhi ya makada wa CCM, wenyeviti wa mikoa na wilaya, wabunge na wafuasi wao wamejiengua na kujiunga upinzani.
Kwa mujibu wa Mzee Moyo, hata waliobaki ni wanaosema wanataka mabadiliko na kuna uwezekano nao wakampigia kura mgombea urais wa upinzani.
Jambo la tatu alilozungumzia kwamba ni kosa ni kitendo cha CCM kuendelea kuongoza nchi kama vile mfumo ni wa chama kimoja.
“Nchi ina historia ndefu… wakati wa kukusanya maoni kuhusu mfumo wa siasa asilimia 80 ya waliohojiwa walitaka mfumo wa chama kimoja na asilimia 20 walitaka vyama vingi. Mwalimu Nyerere kwa upeo wake alishawishi watu waliotaka chama kimoja wakubali mfumo wa vyama vingi na ndipo CCM walikubali vikarejeshwa vyama vingi,” anasema Moyo.
“Lakini CCM waliokubali mfumo wa vyama vingi wanamwona mpinzani kama adui jambo ambalo ni kosa kubwa. Sisi si adui, tofauti za itikadi zisitujengee uadui; mpinzani si adui,” anasisitiza.
Mwanasiasa huyo aliyewahi kuwa waziri katika Baraza la Mapinduzi Zanzibar na waziri katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano anasema jambo la nne ambalo ni tishio kwa CCM ni kuongezeka kwa mwamko wa mabadiliko kwa vijana na wazee hadi vijijini.
“Wiki iliyopita nilikuwa Songea, katika vijiji vingi nilivyopita vijana wanataka mabadiliko na wazee wanataka mabadiliko. Vijijini ilikuwa ngome ya CCM kwa miaka mingi, lakini sasa upinzani umeingia,” anasema.
Moyo anasema anapozungumza na vijana wanamwambia wanataka mabadiliko kutoka kwa watu walioko nje ya chama siyo ndani ya chama. “Wanasema iwe isiwe tunataka mabadiliko,” anasema akinukuu kauli za vijana aliozungumza nao katika vijiji vya Mpitimbi, Songea na akaongeza: “Siyo vijijini tu na hata mjini mwamko umeongezeka.”
Hivyo, Mkongwe huyo anasema haoni uwezekano wanaotaka mabadiliko kudanganyika kwa kauli za kwamba mabadiliko ya kweli yatatoka ndani ya CCM kwani hao wanaoambiwa si watoto, wengine wamekuwapo kwa zaidi ya miaka 50 hawajaona mabadiliko.
Jambo la tano linalomfanya aupe upinzani nafasi ya kushinda anasema ni kuimarika kwa upinzani. Kwamba japokuwa vyama vinavyounda Ukawa vimekuwa na tofauti za sera na itikadi vimefanikiwa kwa kiasi kikubwa kushikamana na kusimamisha mgombea mmoja katika majimbo mengi ya ubunge na kata kwa ajili ya madiwani.
“Tofauti kati yao lazima zitatokea lakini angalia dhamira yao, wamefanikiwa kusimamisha mgombea mmoja katika majimbo mengi; tofauti hazijawazuia, wanasonga mbele,” anasema na kusisitiza kwamba chini ya Ukawa anaona CUF ni imara zaidi Zanzibar.
Aprili mwaka huu alipohojiwa na mwandishi wa makala hii, aliwataka wana CCM kujifunza historia ya chaguzi zilizopita kuanzia ule wa mwaka 1963 ambao ASP ilijinasibu kuwa itashinda na ikapeleka hivyo ujumbe kwa Mwalimu Nyerere, lakini muungano wa ZNP na ZPPP ndio ulishinda.
“Lakini historia ya leo inaonyesha Pemba nzima iko chini ya CUF, CCM haiko kule iko Unguja tu ambako CUF imeanza kushinda viti. Tunatumia sana hisia kwamba tutashinda, dhana hii ni potofu,” anasema.
Jambo la sita linalomfanya aupe upinzani nafasi ya kushinda ni mvuto wa mgombea urais wa Ukawa, Edward Lowassa kuungwa mkono na watu wengi.
“Tumuombe Mungu mambo yaende vizuri, tumekubali chaguzi za vyama vingi tufuate taratibu zake. Mwaka huu ni wa mshituko. Watu hawakutarajia. Mgombea wa Ukawa ameshtua watu. Wanamfuata kwa makundi tangu akiwa ndani ya CCM,” anasema.
“Watu wanamfuata Lowassa; wanafuata mabadiliko. Wanamwona Lowassa kama alama ya mabadiliko siyo Magufuli wa CCM. Huwezi kufanya mabadiliko ukiwa ndani ya CCM lazima utoke nje,” anaeleza.
Mwisho, anasema CCM wanaweza kuanguka kutokana na kosa la kimkakati kwamba wanategemea sana vitisho vya kisiasa. “Utasikia, ‘tutashinda kwa asilimia 90’ kama vile hakuna upinzani, labda miaka ya nyuma lakini si mwaka huu.
Kule Marekani, zilitumika hila kuhakikisha Barack Obama hashindi lakini vijana wa Marekani wakasema, ‘tunataka mabadiliko’ wakampa kura akashinda. Nionavyo Watanzania wanataka mabadiliko kutoka nje ya CCM,” anasema.
Ushauri
Moyo ambaye alifanikisha maridhiano kati ya CCM na CUF Zanzibar akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano ameshauri watu wakapige kura kwa amani na utulivu na kwamba waliopewa dhamana ya kusimamia uchaguzi NEC na ZEC wasimamie viapo vyao maana ni katika viapo hivyo “waliomba Mungu awasaidie wasipindishe haki.”






SOURCE:Mwananchi





































Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

USAJILI WENYE MANUFAA EPL HADI SASA..